Tafuta katika Blogu Hii

Tafuta katika Blogu Hii

Alhamisi, 3 Septemba 2020

Historia ya mzee jumbe

Historia ya AL-HAJI ABOUD JUMBE MWINYI 

Mwasisi wa serikali tatu Tanzania

Na Yahya Abdullah Khamis (Yahya MAKAMO)

Namfananisha Aboud Jumbe Mwinyi na  aliyekuwa Rais wa Urusi (1990 – 1991), Mikhail Gorbachev, mwanzilishi wa sera ya ‘Glasnost (sera ya uwazi) na Perestroika—mfumo mpya wa kisiasa na kiuchumi.

Gorbachiev alipojaribu kuleta sera hiyo, alipingwa vikali na wahafidhina ambao walizoea kuhodhi madaraka na upangaji wa mambo ya biashara, uchumi na kuikandamiza demokrasia.

Pamoja na Jeshi la Urusi kumpindua na kumweka kizuizini, Gorbachev alirejeshwa madarakani kwa nguvu ya wananchi ambao walifanya maandamano ya kumunga mkono.

Jumbe aliteuliwa kushika nafasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, baada ya kuuawa kwa Rais Abeid Amani Karume, mnamo Aprili, 1972.

Alianza kuonesha nia ya mabadiliko mara alipoingia madarakani kwa kuachana na siasa na sera za mabavu za mtangulizi wake na kuwafanya wananchi wa Zanzibar waanze kupumua na kujisikia huru zaidi.

Rais Jumbe ndiye aliyeleta Katiba ya Zanzibar (1979) baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Katiba ambayo ilitenganisha madaraka ya Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi.

Jumbe akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alizindua kwa mara ya kwanza, Baraza la Wawakilishi na kufungua milango ya uhuru kwa Wazanzibari ambapo mtangulizi wake Karume, alitawala kwa Amri (Decree) za Baraza la Mapinduzi na kulikuwa hakuna mwenye ubavu wa kuhoji.

Kabla ya kuwa Rais, Jumbe, alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe na alishika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa ni pamoja na ile ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar baada ya Khasim Hanga, aliyekuwa anashikilia wadhifa huo, kupotea katika mazingira tatanishi.

Wakati wa mauaji ya Karume, Jumbe alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Muungano).

Baada ya uchaguzi wa kwanza wa Zanzibar 1985, Jumbe alichaguliwa na kuhalalishwa kuwa Rais wa Zanzibar, wadhifa ambao pia ulimpa nafasi ya kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Mwenyekiti wa Afro-Shirazi Party (ASP).

Kwa nyadhifa hizo na kufuatana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, moja kwa moja akawa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Kwa ufupi Jumbe, ambaye aliaminiwa sana na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere hata kumtuma kumwakilisha kwenye mikutano ya kimataifa, alikwaa kisiki na kumtibua nyongo Nyerere alipoanza kujihusisha zaidi na masuala ya dini.

Nyerere alikuwa anapinga jambo hili kwamba viongozi wa juu wa Serikali wasijihusishe na mambo hayo kwa kuwa Katiba inatamka kwamba Serikali haina dini.

Baada ya kuviunganisha vyama vya ASP na TANU (Tanganyika African National Union), Jumbe kwa nafasi yake ya Rais wa Zanzibar, pia akawa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, lakini mnamo mwaka 1984, katika kile kilichoitwa na CCM, uchafuzi wa kisiasa wa hali ya hewa Zanzibar, alilazimishwa kujivua nyadhifa zote katika Chama na Serikali. Kosa lake kubwa ni kuhoji muundo wa Muungano.

Hadi anafariki dunia, Mzee Jumbe, ambaye baada ya kuvuliwa uongozi, hakuruhusiwa kurudi Zanzibar, alikuwa muumini wa Serikali Tatu na maandishi yake yanadhihirisha hivyo.

Alitengeneza mashitaka akisaidiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bashir K. Swanzy, raia wa Ghana na kutaka kuyapeleka kwenye Mahakama ya Katiba kama inavyotamkwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, akionesha kuwa 1+! = 3. Mantiki yake ikiwa: ni kuna nchi huru mbili zilizoamua kuungana, zikazaa nchi inaitwa Tanzania—Zanzibar ipo, inaonekana, mbona Tanganyika haipo, iko wapi? Kiurahisi ni kwamba mke na mume wanapoana, wakizaa mtoto, familia ina kuwa ya watu watatu! Hati ile ya mashtaka haikuona mwanga, ilipotea na kutua mezani kwa Rais Nyerere.

Aidha, kama ule upotevu wa document ya Mashitaka haukutosha, Mzee Jumbe akaandika barua kwenda kwa Mwalimu Nyerere akionyesha kuwa Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, vilikuwa vimekiukwa na akataka pia vyama vilivyokuiwa vinatawala kabla ya Muungano, yaani TANU na ASP virudi—kila kimoja upande wake. Hii ilitafsiriwa kwamba Alhaj Aboud Jumbe alikuwa na nia ya kuvunja Muungano.

Barua hiyo, kama ile Hati ya mashitaka, iliibiwa mezani kwa Rais wa Zanzibar na kumfikia Mwalimu Nyerere. Mizengwe na mikwara iliyofuata kwenye Halmashauri Kuu ya CCM, hatimaye ikamwondoa Mzee Jumbe katika ulingo wa siasa Tanzania.

Suala la glasnost na perestroika lilipoibuka ndani ya CCM na Wajumbe wa Baraza la Katiba, kidogo wakabane makoo upande mmoja ulipohoji Mkataba wa Muungano na Sheri ya Muungano—mambo ambayo alihoji Mzee Jumbe mwaka 1984.

Wakati wa kutafuta maoni kupitia Tume ya Jaji Joseph Sinde Warioba, viongozi karibu wote kutoka Zanzibar na taasisi zake, walipendekeza kubadilika kwa Muungano kuwa Serikali Tatu kama ilivyokusudiwa katika hati ya Muungano, yaani kuwe na Serikali ya Tanganyika yenye madaraka kamili na kuwe na Serikali ya Zanzibar yenye madaraka kamili. Juu ya serikali hizi mbili iwepo Serikali ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe wa Baraza la Katiba kutoka Zanzibar, ambao walijiapiza kwamba safari hii hawatakubali kuondoka Dodoma na kurudi Zanzibar bila Zanzibar yao. Wakasema Zanzibar inazidi kupotea kwa kuwa mambo mengi ambayo hayakuwa ya Muungano, yameongezwa kinyemela na ndio yanachangia kuidhoofisha Zanzibar. Kwenye Hati ya Muungano kulikuwa na mambo 11 tu na ndio waliyotaka yabaki, walitaka mengine 15 yaliyoongezwa yaondolewe.

Cha kushangaza ni kwamba, walipofika Dodoma hali ya hewa na hoja madhubuti za upinzani ambao walitaka Serikali Tatu vikawachanganya, wajumbe wa CCM kwenye Baraza la Katiba, ikiwa ni pamoja na wajumbe waliojiapiza wakati wanaenda Dodoma kwamba safari hii hawatakubali kuburuzwa na Bara, sauti zao zikafifia na mwisho kupotea kabisa.

Miguu yao ikaota matende, wakashindwa kuandamana kama walivyofanya Warusi, kumwunga mkono Rais wao Gorbachev, wakashindwa hata kutaja jina la Aboud Jumbe kwenye hotuba zao!

Hii ilitokana na ukweli kwamba wajumbe kutoka Zanzibar, wangekomalia hoja ya Serikali Tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Warioba, wangeonekana kwamba wanaungana na wapinzani na CCM ingeangamia.

Ikumbukwe kwamba mwaka huo ulikuwa wa Uchaguzi Mkuu na kisiasa Chama Cha Mapinduzi kilikuwa hakiko vizuri. Kulikuwa na dalili zote za kukipoteza kama kilivyopotea katika duru za siasa chama kilichokuwa kinatawala nchini Kenya—Kenya African National Union.

Alhaj Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, ameaga dunia akiwa na umri mkubwa wa miaka 96 akiwa amepanda mbegu ya mageuzi na demokrasia, japo ameondoka bila kuyaona matunda ya harakati zake, tofauti na Nelson Mandela wa Afrika Kusini ambaye ameiacha nchi yake ikiwa huru na imeondokana na siasa chafu ya ubaguzi wa rangi, historia itamdhirisha kwamba alipigania haki ya Wazanzibari.

Usiache kuendelea kufuatilia blog hii

Ijue Historia ya Pemba kiundani

 

KISIWA CHA MARASHI YA KARAFUU


Na  YAHYA ABDULLAH KHAMIS (MAKAMO)


Neno Pemba lina asili na maana tofauti.
Pemba ni jina maarufu sana la mtoto wa
kiume hukoTibet likimaanisha “ aliyezaliwa
Jumamosi”. Kuna Mji ujulikanao kama Pemba
huko Msumbiji. Ipo nadharia inayodai kwamba
ni jamii ya wamakonde wa Msumbiji wa eneo
hili waliokwenda katika kisiwa cha Pemba
kuhamia na kuanzisha jamii ya wapemba.
Neno Pemba pia liko miongoni mwa watu wa
kusini ya Mali ambao wanajulikana kama
Mandika. Kwa mujibu wa imani za kijadi za
Mandika, Mungu Mangala ameumba ulimwengu
(binadamu na ardhi) kutokana na mapacha
wawili (Pemba na Farro) waliokuwemo katika
yai hapo mwanzoni. Pemba, mmoja wa
mapacha hao alijaribu kutoka katika yai huku
akiiba kipande cha yai (mama yake) na
kukirusha angani Baada ya kitendo hichi kile
kipande cha yai kilichobaki kikawa ardhi.
Mungu Mangala akamgeuza Farro kuwa
mwanadamu na sehemu iliyobaki ya yai
akaigeuza kuwa jua (yaani chanzo cha
mwanga). Pemba akamgeuzwa kuwa giza
lililoambatana na usiku. Kwa hivyo kwa mujibu
ya imani za kitamaduni za watu hawa waMali,
Pemba nigiza la usiku. Hwenda ikawa jina
limesibu maana historia ya siasa ya nchi tokea
miaka ya 1960 kisiwa hichi kilikuwa katikagiza
nene.
Pia neno Pemba linadaiwa na baadhi ya wazee
wa kisiwa hichi kuwa na asili yake katika neno
pee au pekeye ikimaanaisha upweke wa
Pemba wa hapo mwanzoni kabisa wakati
kisiwa hichi kilipojitawala peke yake bila ya
mafungamano na sehemu yoyote. Bila shaka
hizo ni zama za kale kabla ya ujio wa wareno.
Mafungamano ya Pemba na Unguja au
sehemu nyengine kiutawala yalianzishwa
baada ya kufika kwa wareno, kuanguka kwa
tawala za Mwinyi mkuu na kuimarika baada ya
utawala wa Mazruyi na Mabusaidi wa Omani.
Nadharia nyengine juu ya asili ya jina hili
Pemba zinaweza kuwepo.
Kisiwa cha Pembakinaoshwa na maji ya bahari
ya hindi, pamoja na kisiwa mwenzake ndugu
cha Unguja kando kidogo ya mwambao wa
Afrika ya mashariki. Pemba ipo katika umbali
wa kilomita 80 kutoka kaskazini ya kaskazini
mashariki (NNE) ya kisiwa ndugu cha Unguja
na halkadhalika kilomita 50 kutoka mwambao
wa Tanzaniabara usawa wa mji wa Tanga.
Katika ramani ya dunia, Pemba ipo baina ya
Latitudo 4 80’ na 5 30’ S, na Longitudo 390
35’ na 390 50’ E. Pemba ina urefu wa maili
40 kutoka kaskazini hadi kusini. Sehemu yake
iliyo pana zaidi kutoka mashariki hadi
magharibi ni maili 10. Ardhi ya kisiwa
chaPemba ni milima na mabonde. Tofauti na
kisiwa mwenzake cha Unguja ambacho kwa
asilia kubwa ardhi yake ni tambarare, kisiwa
chaPemba kwa asilimia kubwa kimeathiriwa na
mabonde kuliko ardhi tambarare. Hivyo basi
hata ujenzi wa miundombinu katika kisiwa
chaPemba unakuwa ni wa tabu na wa
gharama kubwa kulinganisha na kisiwa cha
Unguja. Minyanyuko inafikia urefu wa futi 600
kutoka usawa wa bahari.
Umbo la kisiwa chaPembani adimu kuonekana
katika visiwa vingi ulimwenguni. Karibu na
bahari, ardhi ya kisiwa hichi imefanya marinda
na kutoa umbile la vidole vinavyoingia masafa
marefu baharini. Sura hiyo imeruhusu eneo
kubwa la bahari kuingia ndani ya ardhi ya
kisiwa hichi na kutoa mandhari mseto ya
kuvutia. Pia uzuri wa mandhari ya kisiwa hichi
umepambwa na mpangilio wa visiwa vidogo
vidogo vilivyopangika katika mstari mmoja
upande wa magharibi wa kisiwa
chaPembakutoka kaskazini ya kisiwa hadi
kusini. Visiwa hivi ni Njau, Fundo, Uvinje,
Kokota, Misali, Makoongwe, Matumbini na
Kisiwa Panza.
Pemba haina idadi kubwa ya wakaazi. Tofauti
na sehemu nyengine za Tanzania ambazo
idadi ya watu huongezeka kwa kiwango
kikubwa sana mwaka hadi mwaka kutokana na
vizazi na uhamiaji, Pemba imeathiriwa sana na
uhamaji wa kasi ambapo wakaazi wake wengi
wanaonekana kutawanyika katika maeneo
mbali mbali nje ya kisiwa hicho kufuatia
ugumu wa maisha, uchumi duni na ufinyu wa
huduma za jamii (agalia jadweli 2).
Jadweli 2:Pembana Idadi ya watu
Mwaka wa
sensa
Idadi ya
watu
Ongezeko (%)
1967 164,321 –
1978 205,304 20
1988 265039 22.5
2002 278,815 5
Ongezeko la idadi ya watu kwa asilimia 5 tu
kutoka mwaka 1988 kuelekea mwaka 2002,
linatofautiana sana na ongezeko la watu la
asilimia 20 kutoka mwaka 1967 kuelekea
mwaka 1978 na lile la asilimia 22.5 kutoka
mwaka 1978 kuelekea mwaka 1988. Hii ni kwa
sababu kutokea miaka hiyo ya 1988 kuelekea
miaka ya 2002 wapemba wamekutana
wakikabiliana na mikiki mingi iliyowapotezea
matumaini ya maisha nyumbani kwao. Hivyo
wakaazi wengi wa kisiwa
chaPembawakakihama kisiwa hicho na kwenda
kutafuta unafuu wa maisha sehemu nyengine.
Kisiwa cha Pemba kwa karne nyingi huko
nyuma kilikuwa kikijulikana kama “ Jaziratul-
khadhraa” yaani kisiwa cha kijani. Katika kitabu
chake cha Zanzibar, The Island metropolis of
Eastern Afrika Pearce anasema hivi: “ Waarabu
waliita Pemba El-Hudhera, au kisiwa cha kijani:
na ni kijani kinachon’gara kama mwangaza wa
kijani unaotokea katika johari, sio kwa
mtazamamo wa kisiasa bali kwa mtazamo wa
kushangaza na kusisimua, ukiangalia kutoka
baharini utaona picha ya kufurahisha ya
minyanyuko ya ardhi, iliyofunikwa na wingi
mkubwa wa uoto wa misitu, mikarafuu,
michungwa na minazi…….milima inayong’aria
kijani ya kisiwa cha Pemba inaanzia mara tu
baada ya bahari, na hili linakipa kisiwa sura ya
mnyanyuko na mandhari mseto, ambayo kwa
kweli imekosekana katika kisiwa ndugu (cha
Unguja)” (Pearce, 1967:306) .
Kama waarabu walivyokiita kisiwa
chaPembakuwa ni ‘kisiwa cha kijani’ basi ndio
hivyo hivyo hali ilivyo. Kisiwa chaPembakina
ardhi iliyo na rutuba na maji ya kutosha. Rangi
ya kijani inayong’ara katika mapori na
mashamba ya mikarafuu inathibitisha kiwango
kikubwa cha rutuba ambacho mpaka sasa
bado hakijaathiriwa na shughuli za uharibfu za
binadamu. Kisiwa kinazo kila aina ya neema
na vyanzo vya uzalishajimalina uimarishaji
uchumi. Kisiwa kimezungukwa na fukwesafiza
mchanga. Vipo visiwa vidogo vidogo ambavyo
navyo vimezungukwa na fukwe za kuvutia na
mandhari ya kupendeza. Ndani ya bahari ya
kisiwa cha Pemba ipo bustani ya kuvutia ya
matumbawe au “coral garden” ambayo huwezi
kuipata katika sehemu zote za dunia.
Inaaminika kwamba zaidi ya asilimia hamsini
za aina zote za matumbawe duniani
zinapatikana kisiwani Pemba, hasa katika
maeneo ya kisiwa cha Misali.
Zao la karafuu ambalo ndio alama kuu ya
kimataifa na umaarufu (international repute)
wa Zanzibar linaonekana kustawi katika
kisiwa cha Pemba. Karafuu ndio rasilimali kuu,
uchumi, na utamaduni wa wapemba. Zao la
karafuu liliingizwa Zanzibarmwaka 1812 na
Bwana Saleh bin Haramil Al-abray, kutoka
katika kisiwa kilichijulikana kama Bourborn
Island, kwa sasa ni Reunion Island . Baadae
Sultan Said bin Sulan akaamua kuipanda
mikarafuu kwa wingi kote Unguja naPemba
kwa kiwango sawa. Kimbunga cha mwaka
1872 kilichozuka Unguja kilipelekea kutoweka
kwa idadi kubwa ya mikarafuu huko Unguja.
Hii ndio sababu mikarafuu inaonekana
kusheheni kwa wingi katika kisiwa chaPemba
kuliko mwenzake Unguja. Ziko pia hadithi
zinazosema kuwa asili ya karafuu ni sanduku
la kichawi aliloletewa zawadi Sultan Said bin
Sultan. Alipolifungua sanduku hilo alikutia
sanduku ndani ya sanduku hadi kufika idadi ya
masunduku saba. Ndani ya sanduku la mwisho
la saba akaona kitu kilichofanana na kokwa za
tende. Kwa kuwa ilikua mara yake ya mwanzo
kuona hakuweza kuelewa kama ni mbegu za
karafuu. Alizipanda mbegu hizo na mikarafuu
ya mwanzo kuanzia hapo.
Karafuu ndio inayofanya chanzo kikuu cha
mapato ya Zanzibarkwa miaka mingi huko
nyuma. Pemba inazalisha asilimia 70 ya
karafuu zote za Zanzibar. Mikarafuu yote
inakisiwa kufika milioni tatu na nusu (350000).
Mkarafuu mmoja unakisiwa kuendelea
kuzalisha karafuu kwa muda wa miaka hamsini
(50). Hapo nyuma kidogo, karafuu za Pemba
ndio zilizokuwa uti wa mgongo wa uchumi wa
nchi yazanzibar. Kwa mfano katika mwaka
1907 Jumla ya mapato ya bidhaa
zilizosafirishwa nje ya nchi ilikuwa £339,000
ambayo ni asilimia 92 ya mauzo yote ya nje.
Pembapia inajivunia fahari kubwa na hazina
muhimu inayopatikana katika kisiwa cha
Misali. Kisiwa cha Misali ni cha aina yake
duniani. Kisiwa kina umbile la msala na hii
ndio asili ya jina lakekuitwamisali. Kwa mujibu
wa jiografia ya ardhi (geology), kisiwa kina
asili yake kutoka katika jabali au jiwe kubwa la
mwamba lililohamiwa na uoto taratibu
(ecological succession) hadi kufikia kuwa na
hadhi ya uoto wa asili wenye miti na wanyama
mbali mbali. Katikati ya kisiwa kuna mapango
makubwa ambayo yamekwenda ndani na chini
kwa chini hadi kukutana na bahari. Pango
kubwa katika hayo ni lile linaloitwa “ kijiwe
bendera cave ” ambalo hujaa maji hadi juu pale
maji yanapojaa baharini na hubakia kavu pale
maji yakitoka baharini. Pango hili linatumika
sana kwa shughuli mbali mbali za kitamaduni.
Mapango hayo ni kivutio kimoja muhimusana
cha utalii ndani ya kisiwa hicho.
Kisiwa cha Misali kinao utajiri mkubwa wa
matumbawe yanayotengeneza bustani ya
kuvutia chini ya ardhi au “coral garden”
ambayo huvutia sana shughuli za uzamiaji za
watalii. Inaaminika kuwa zaidi ya asilimia 50
za aina ya matumbawe ya Afrika mashariki na
duniani kiujumla yanaonekana katika kisiwa
cha misali pekee. Kisiwa pia kinao utajiri
mkubwa wa samaki waliosheheni kwa wingi na
waliohifadhika kwa karnne nyingi. Hata
nyangumi wamesheheni katika bahari za
kisiwa cha misali.
Pembapia inao utajiri wa misitu. Hadi katika
kipindi cha katikati ya karne ya 19 karibu ardhi
yote ya Pembaimenfunikwa na misitu. Baada
ya hapo tena misitu mingi ilifyekwa kwa ajili
ya upandaji wa mikarafuu. Hata hivyo Pemba
bado mpaka sasa inayo hifadhi kubwa ya
misitu. Msitu mkubwa ni msitu wa ngezi ulioko
katika wilaya ya Micheweni. Ijapokuwa msitu
upo karibu na pwani bado unao mchanganyiko
wa miti wa aina ya peke yake Afrika ya
Mashariki. Miti ya Asia ya mashariki na hata
Madagascar ipo katika msitu wa ngezi. Miti hii
ni kama vile Musa acuminata na Yyphanodorum
lindleyanum. Miti mingi iliongezwa kwa
kupandwa lakini pia ipo miti mingi
inayoshangaza kuwepo kwake. Msitu wa ngezi
una miti yake na wanyama wake pia ambao
huwezi kuwaona sehemu yoyote duniani.
Katika msitu wa ngezi wanaonekana popo
wasiopatikana duniani kote. Popo hawa,
Pembaflying foxes, au Pteropus Voeltzkowi ni
wakubwa na wana manyoya ya rangi nyekundu
kifuani. Mbali ya popo huyu adimu, ndani ya
msitu wa ngezi kuna wanyama wengine ambao
pia ni adimu sana duniani. Wanyama hawa ni
kama vile kima wa Pemba (Pemba vervet
monkey) au Cercopithecus nesiotes na Kima
punju (Red colobus) au Colobus badius
aliyeletwa msituni hapo kutokea Unguja katika
mwaka wa 1970. Nyati wa rangi ya buluu au
Cephalopus monticola pembae pia anapatikana
katika msitu wa ngezi tu . Msituni wapo pia
nguruwe (Ferel pigs) au Sus scrofa ambao
waliletwa msituni hapo na wapotugizi kutokea
kwao Ureno. Miti na wanyama wengi wengine
wapo katka msitu huo ambao ni hazina
muhimusana kwa kisiwa chaPemba.
Pia tafiti za miaka mingi huko nyuma na hata
za hivi karibuni zinaonyesha kuwepo kwa
utajiri mkubwa wa mafuta na gesi asilia katika
bahari na ardhi za kisiwa hichi. Japo kuwa
mafuta yameripotiwa kuwepo pia katika kisiwa
ndugu cha Unguja, taarifa za uhakika
zinaonyesha mafuta haya yapo kwa wingi zaidi
katika kisiwa chaPemba. Suala la mafuta
ambayo bila kigugumizi chochote yamesheheni
katika bahari na ardhi zakisiwa cha Pemba
limekuwa chanzo cha fitina na malumbano ya
masuala ya muungano baina
yaZanzibarnaTanganyika. Pia tafiti za zamani
zinathibitisha kuwepo kwa kiwango Fulani cha
dhahabu katika kisiwa chaPemba.
Pembaimejaaliwa wingi wa rasilimali na
neema mbali mbali zilizo bora. Kwa wafanya
biashara wa bidhaa za hapa nyumbani kwa
wao bidhaa bora ni zile zitokazoPemba. Ndio
maana unasikia halua ni ya Wete Pemba
bwana! Imekuwa bidhaa yenye kutoka Pemba
ndio iliyo na soko zaidi na ndio inayonunuliwa
zaidi ndani yaZanzibar. Imekuwa ni jambo la
kawaida sasa kwa wafanya biashara kutumia
hadaa ya jina la Pemba kuuza bdhaa zao hata
kama hazitokiPemba. Ukipita mitaani utasikiaa
muhogo wa Pemba na asali ya Pemba.
Ungana nami katika blog yangu kuendelea kujuzana historia zetu zaidi.
Ahsante.






Tuingalie Historia Ya Seif Sharif Na Aboud Jumbe Mwinyi

 " SIKUMMALIZA SHEIKH ABOUD JUMBE MWINYI – "Maalim Seif"

Hio ni nukuu ya Maneno ya Maalim SEIF SHARIF HAMAD juu ya maisha ya hayati mzee ABOUD JUMBE MWINYI

Mwaka 1984, Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Makamo wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aboud Jumbe Mwinyi, alilazimishwa kujiuzulu katika Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma akishutumiwa kutaka kuvunja Muungano. Kitendo hiki kimekuwa kikichukuliwa na Wazanzibari kama udhalilishaji mkubwa kwa nchi na heshima yao, na msimamo wa serikali tatu, ambao Jumbe anasemekana kuutetea umekuwa ndio msimamo wa Wazanzibari. Kujiuzulu kwa Jumbe kunaunganishwa na tafauti za kimtazamo baina yake na Katibu Mkuu wa sasa wa ACT WAZALENDO Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye hata hivyo anasisitiza katika makala hii kwamba hajawahi kutafautiana na Jumbe kuhusu mtazamo wa Muungano.

Kwanza niweke kumbukumbu sawa. Mwaka 1984 wakati Mzee Aboud Jumbe anajiuzulu nyadhifa zake zote, mimi ni kweli nilikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa [NEC] ya CCM, na hivyo kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi. Hata hivyo wakati huo sikuwa miongoni mwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi. Kwani nilikuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1980. Nikateuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar na Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeteuliwa kuwa Rais wa Muda wa Zanzibar mara baada ya Mzee Aboud Jumbe kujiuzulu mwaka 1984. Hivyo kuanzia mwishoni mwa 1980 hadi mwanzoni mwa 1984 sikuwa kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi.

Pili, tangu Chama cha Wananchi CUF kiasisiwe hapo 1992, sera yake rasmi ni kuwepo kwa Muungano wa serikali tatu: yaani Serikali ya Muungano, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika.

Pengine itakumbukwa kuwa hata Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema kuwa Chama cha Siasa chochote kile kina haki ya kuwa na sera yake juu ya Muungano. Akasema kuwa kama vile ni haki ya CCM kuwa na sera ya serikali mbili kuelekea serikali moja, CUF wanayo haki hiyo hiyo ya kuwa na sera ya serikali tatu katika Muungano. Mwalimu Nyerere akamalizia kwa kusema kuwa na sera juu Muungano inayotafautiana na sera ya CCM si uhaini. Waachiwe wananchi waamue!

Hivyo basi msimamo wangu tangu kuasisiwa kwa Chama cha Wananchi, CUF haujapata kubadilika. Ni msimamo na sera ya Chama changu cha CUF. Sera ya kuwepo kwa serikali tatu katika Muungano wetu.

Hivyo niseme, kama nilivyokuwa nikisema kila nilipopata nafasi, kuwa bila ya kuubadili muundo wa Muungano wetu kutoka muundo wa sasa wa serikali mbili kwenda kwenye muundo wa serikali tatu, matatizo ya Muungano yataendelea kuutafuna Muungano wetu. Badala ya kuuimarisha tutakuwa tunaendelea kuudhoofisha. Kuimarisha Muungano sio kuongeza orodha ya Mambo ya Muungano katika Katiba. Hili linadhoofisha Muungano. Kwani nguvu za Muungano zitatokana na wananchi wa pande mbili kuukubali kwa dhati Muungano wenyewe. Kuhakikisha kuwa wananchi wa pande zote mbili wanaridhika na muundo wake, mamlaka na madaraka ya kila upande na serikali yake. Na zaidi kuliko yote, wananchi wa pande zote mbili kuridhika kuwa wanatendewa haki katika Muungano.

Vyenginevyo tutakuwa tukibadili misamiati tu: mara tutayaita matatizo ya Muungano; mara tuziite kero za Muungano, pengine tutakuja kuyaita mapungufu ya Muungano, au hata bughdha za Muungano, na kadhalika.

Suala la kutoka serikali mbili kwenda serikali moja hilo halitakubalika. Mimi silikubali. CUF hailikubali, na Mzanzibari mzalendo yeyote halikubali. Siamini kuwa Serikali ya Muungano itakuwa tayari kutumia vifaru, mizinga na madege ya kivita kulazimisha muundo wa serikali moja.

Baada ya kuweka msimamo huo, sasa nigeukie mambo mengine uliyoniuliza.

Kwamba Mzee Aboud Jumbe alituhumiwa kutaka kuwepo kwa muundo wa Muungano wa serikali tatu na akalazimishwa kujiuzulu. Wakati huo mimi nilitetea muundo wa sasa wa serikali mbili.

Ili hili lifahamike vyema na wananchi ni vyema kwanza kuelezea mazingira yaliyomfikisha Mzee Aboud Jumbe kujiuzulu.

Nitangulie kueleza kuwa mimi binafsi na kwa dhati ya nafsi yangu namuheshimu na namthamini sana Mzee Aboud Jumbe. Kwanza ni mwalimu wangu nilipokuwa nasoma katika skuli ambayo wakati huo ikiitwa The King George VI Secondary School (sasa Lumumba College).

Pili, ni Mzee Aboud Jumbe ambaye alisababisha mimi kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara baada ya yeye kuwa Rais wa Zanzibar mwaka 1972, baada ya kukaa kwa miaka minane (8) tangu nilipomaliza masomo ya Kidatu cha Sita (Form VI) hapo 1963 na kuzuiwa na Serikali ya Mapinduzi kujiunga na masomo ya Chuo Kikuu, pamoja na kuwa kila mwaka nilikuwa napata nafasi katika vyuo mbali mbali duniani.

Tatu ni Mzee Aboud Jumbe huyo huyo aliyesababisha mimi kuwa kiongozi katika Serikali ya Mapinduzi na kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa CCM. Hivyo namshukuru na katu siwezi kumsahau kwa mchango wake mkubwa ulionifanya nilivyo.

Sasa nirejee kuelezea mazingira ya wakati huo ambayo yalikuwa kama ifuatavyo:

Nianzie mwaka 1982 ambapo kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa CCM. Katika kipindi kilichotangulia Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM wa 1982 wa kuchagua viongozi wa kitaifa, kulijitokeza makundi mawili miongoni mwa viongozi wa CCM kutoka Zanzibar yaliyokuwa yakikinzana. Kundi la kwanza likijulikana kama Liberators, na la pili likijulikana kama Frontliners. Kundi la Liberators kimsingi lilikuwa na viongozi ambao walikuwa wanapinga mabadiliko ya aina yoyote yale katika uendeshaji wa mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Zanzibar.

Kwa lugha ya sasa unaweza ukaliita kundi la Wahafidhina. Kundi la Frontliners lilikuwa na vijana, damu mpya iliyoingia katika uongozi wa Chama na SMZ. Kundi hili lilitaka mabadiliko katika uendeshaji wa mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Unaweza ukaliita kundi la Reformers.

Uchaguzi wa viongozi wa kitaifa (Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa) wa 1982 ulishuhudia msuguano mkali kati ya makundi hayo mawili. Nia ya Liberators ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Frontliners hawaingii katika Halmashauri Kuu ya Taifa. Nia ya Frontliners ilikuwa ni kuhakikisha damu mpya inaingia katika kikao hicho kikuu cha maamuzi cha Chama ambacho wakati huo kilikuwa ndio kimeshika hatamu zote za uongozi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Bahati njema Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM, kwa busara zake, uliwaingiza watu kutoka makundi yote mawili katika NEC na, baadaye, NEC ikawaingiza watu kutoka makundi yote mawili katika Kamati Kuu.. Frontliners walishukuru kuona kuwa miongoni mwao walifanikiwa kuchaguliwa kuingia katika vikao vyote viwili vikuu vya maamuzi vya Chama.

Kwa upande mwengine, Liberators hawakufurahi. Liberators hao walishaweka shinikizo kwa Mzee Aboud Jumbe (ambaye ndiye chanzo cha kuingiza damu mpya katika CCM ya wakati huo) kuwa vijana aliowaingiza watakujamgeukiana kuwaondoa wao, Liberators, na yeye mwenyewe katika uongozi. Inaelekea Mzee Aboud Jumbe alishawishika na shinikizo hilo, na hivyo naye, kwa njia zake (nyuma ya pazia), alitaka kuona kuwa Frontliners hawaingii katika NEC na Kamati Kuu ya Chama ambako pengine wangekuwa na ushawishi katika maamuzi ya sera za Chama. Frontliners walipoingia, ikawalazimu Liberators na Mzee Aboud Jumbe kutafuta njia nyengine ya kuweza kuwazingira ili, ikiwezekana, waweze kuondolewa katika ramani ya uongozi wa Chama na Serikali.

Hivyo basi, mara baada ya kikao cha Mkutano Mkuu wa Taifa kumalizika mwezi Novemba, 1982, Mzee Aboud Jumbe aliwataka Wajumbe wote wa NEC kutoka Unguja akutane nao Unguja, na Wajumbe wote wa NEC kutoka Pemba akutane nao Pemba. Katika mikutano hiyo, hotuba ya mwalimu wangu, Mzee Aboud Jumbe, ilitushtua wengi. Mzee Aboud Jumbe alishtumu kuwa kuna watu wanaoleta uchochezi kutaka kuvigawa visiwa vya Unguja na Pemba; kutaka kuigawa mikoa, yaani mkoa mmoja dhidi ya mwengine katika kila kisiwa; kutaka kuzigawa wilaya, yaani wilaya moja dhidi ya nyengine katika kila mkoa; na kutaka kuvigawa vijiji, yaani kijiji kimoja dhidi ya chengine katika kila wilaya. Akamalizia kwa kusema kuwa watu hao watahukumiwa na kuonja kile alichokiita “Revolutionary Justice”

Hili lilitushtua wengi, hasa sisi vijana wa wakati huo. Tukakumbuka historia ya Zanzibar tangu Mapinduzi ambapo watu walioshukiwa kuwa wapinzani wa serikali, na hasa wasomi, walivyoshughulikiwa kwa kuhakikisha kuwa wanatoweka kabisa. Khofu yetu ikawa jee, hawa wazee si wamekusudia kuturudisha huko huko tulikotoka? Tukasema kama hatukuchukua hatua za kichama kulizuia hili, basi kuna uwezekano wa historia kujirudia na watu wasiokuwa na hatia kupotea kwa kile kinachodaiwa kusimamisha “Revolutionary Justice”

Hivyo baadhi yetu tuliokuwa Wajumbe wa Sekretariati ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama, hasa sisi kutoka Zanzibar, tukamfuata Mzee Rashid Kawawa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM na Mwenyekiti wa Sekretarieti na kumueleza khofu yetu hiyo. Mzee Kawawa akatuelewa na akaamua iletwe agenda juu ya suala hilo katika kikao 
kilichofuata katika Sekretarieti. Agenda ikaletwa. 

Ikajadiliwa kwa mapana yake, kisha ikawasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu. Kamati Kuu ikaamua kuunda timu mbili kwenda kuchunguza madai yale
            Mwandishi : YAHYA ABDULLAH KHAMIS (MAKAMO)










HISTORIA YA MAISHA YA ALI HASSAN MWINYI NA NYADHIFA ZA UONGOZI ALIZOSHIKA

 

HISTORIA YA MZEE RUHSA


AL-HAJJ ALI HASSAN MWINYI

Mwandishi :Yahya Makamo

LEO KATIKA HISTORIA:  TUMJUE  "MZEE WA RUKHSA" RAIS MSTAAFU ALI HASSAN MWINYI


Ali Hassan Mwinyi alizaliwa tarehe 8 mwezi wa tano (Mei) mwaka 1925 katika kijiji cha Kivure, wilayani Kisarawe ,mkoa wa Pwani, Tanzania Bara. Kama wengi wa viongozi wetu, Mwinyi naye alizaliwa katika iliyokuwa Tanganyika. Akiwa bado mwenye umri mdogo sana familia yake ilihamia Zanzibar. Kwa maana hiyo Mwinyi ni mzaliwa wa bara aliyekulia na kuendelea kuishi visiwani Zanzibar.


Alianza safari yake kielimu huko visiwani Zanzibar katika shule ya msingi Mangapwani kuanzia mwaka 1933 hadi 1936 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari Dole kwa ajili ya elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1937 mpaka mwaka 1942. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Cha Ualimu Zanzibar kusomea ualimu kuanzia mwaka 1943 mpaka 1944.


Kuanzia mwaka 1945 mpaka mwaka 1950 alirejea tena katika shule ya Mangapwani,shule aliyosomea,safari hii akiwa sio mwanafunzi tena bali Mwalimu.Kuanzia mwaka 1950 mpaka 1954 alikuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo wakati huo huo alikuwa akiongeza elimu yake kwa kujipatia General Certificate in Education (GCE) na pia aliendelea kusoma chuo cha Durban University Institute of Education, United Kingdom kusomea stashahada ya ualimu.

Baada ya hapo alijiunga tena na Chuo Cha Ualimu Zanzibar kama mkufunzi kuanzia mwaka 1956 mpaka mwaka 1961 Pia alirudi Regent Institute kilichopo London nchini Uingereza ambapo alijipatia cheti cha ufundishaji lugha ya kiingereza.


Kuanzia mwaka 1961 mpaka 1962 alijiunga na Hall University, Uingereza katika Tutors’ Attachment Course. Mzee Mwinyi pia ana cheti ya lugha ya kiarabu alichokipatia Cairo nchini Misri kati ya mwaka 1972 na 1974.


Safari yake ya kisiasa aliianza rasmi mwaka 1964 alipojiunga na Afro Shiraz Party (ASP) huko Zanzibar ambapo alikitumikia chama katika ngazi na nafasi mbalimbali.

Kati ya mwaka 1964 na 1965 alikuwa ni Katibu Mkuu wa muda katika wizara ya elimu Zanzibar kabla hajateuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi katika iliyokuwa Zanzibar State Trading Corporation (ZSTC).

Hiyo ilikuwa ni kati ya mwaka 1965 na mwaka 1970. Pia katika miaka hiyo hiyo, kuanzia mwaka 1966 mpaka 1970, Mwinyi alikuwa mweka hazina msaidizi katika tawi la ASP la Makadara,Zanzibar. Wakati huo huo pia kati ya mwaka 1964 mpaka 1977 alikuwa ni mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)


Majukumu mengine aliyokuwa nayo miaka hiyo ni pamoja na uenyekiti wa Zanzibar Censorship Board (1964-1965), Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na pia mwenyekiti wa Baraza la Chakula na Lishe.


Kuanzia mwaka 1972 mpaka 1975, Mwinyi alikuwa ni Waziri wa Afya wa Tanzania kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kuanzia 1975 mpaka 1977. Mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri cheo alichokitumikia mpaka mwaka 1982 aliporejea nyumbani na kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii cheo ambacho alikutumia kwa muda mfupi tu kwani mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi katika ofisi ya Makamu wa Raisi.


Mwaka 1984, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Raisi wa Zanzibar wakati huo,Alhaj Aboud Jumbe, Mwinyi alichaguliwa kuwa Raisi wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na wakati huo huo Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Kuanzia mwezi August mwaka huo huo wa 1984 Mwinyi alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi cheo alichoendelea nacho mpaka mwaka 1990 baada ya kung’atuka kwa Hayati Mwalimu Nyerere kutoka katika kukiongoza Chama Cha Mapinduzi(CCM)


Mwalimu Nyerere aliamua kung'atuka kwa hiari yake na kumuachia kwa njia ya kidemokrasia madaraka ya urais Alhaji Ali Hassan Mwinyi. Hiyo ilikuwa mnamo 1985.


Alipoingia madarakani kumpokea aliyekuwa Raisi wa Awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Nyerere mnamo tarehe 5 Novemba mwaka 1985, watanzania wachache sana (kama wapo) waliweza kutabiri kwamba miaka kumi baadaye na zaidi baada ya kustaafu rasmi, ataibuka kuwa mmojawapo wa maraisi wa Tanzania ambao watabakia kupendwa na kuheshimika kwa namna ya kipekee kabisa.


Tunadiriki kusema “namna ya kipekee” kwa sababu ukweli unabakia kwamba inapofanyika tathmini ya uongozi wake, bado mtu au watu mbalimbali wanakuwa na maoni yao tofauti tofauti kuhusiana na suala hilo. Utoaji huo wa tathmini ni suala ambalo haliwezi kukoma leo wala kesho, ni tukio linaloendea na litakaloendelea, vizazi mpaka vizazi.


Mwinyi kihistoria na utawala wake.


Huo ndio uzuri au ubaya wa historia na muda (history and time),huwa vina jinsi ya kipekee katika kutoa hukumu zao.


Mpaka anakabidhi madaraka yake ya uraisi kwa raisi wa awamu ya tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa mnamo tarehe 23 November mwaka 1995, jina ambalo wengi tulipenda kulitumia ni “Mzee Rukhsa” ingawa kamwe hatukuwahi kusahau kwamba jina lake kamili ni Ali Hassan Mwinyi, Raisi wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.


Kihistoria, Ni wakati wa Uongozi wake ndipo mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa!


Rais Msaafu wa awamu ya pili Mh. Ali Hassan Mwinyi ni mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na pia hupenda michezo hususani jogging. Mwinyi ameoa wake wawili (Sitti Mwinyi na Khadija Mwinyi)

 ana watoto na wajukuu. Anaishi Msasani jijini Dar-es-salam




 











 









HISTORIA YA KISIWA CHA PEMBA NA WATU MASHUHURI

YAHYA ABDULLAH KHAMIS

HISTORIA YA PEMBA
Ndugu Wazalendo, Wazanzibari na wananchi
wenye asili ya Pemba kwa ujumla.
Hivi karibuni, nilikuwa kisiwani Pemba kufanya
utafiti wa masuala mbali mbali yahusuyo mila
na utamaduni wa watu wa Pemba.
Moja kati ya mambo yaliyonivutia sana ni pale
nilipogundua kuwa kuna watu kutoka katika
kisiwa hicho kidogo ambao ni maarufu, wenye
nguvu, na wenye kuheshimika zaidi na baadhi
yao ni wenye kuogopwa sana kwa sababu
moja au nyengine. Kikubwa zaidi, ni kuwa
umashuhuri wa watu hao unaendelea hata
kama watu hao ameshafariki miaka thelathini
au hata karibu karne moja nyuma.
Kuna sababu nyingi zinazowafanya watu wawe
mashuhuri, wenye nguvu, wanaoheshimika na
hata kuogopesha katika jamii zao kiasi
kwamba umashuhuri wao huo huvuuka viunga
vya miji yao na kujulikana mbali zaidi ya
maeneo yao hayo. Miongoni mwa sababu
zinapolekea umashuhuri huo ni cheo au uluwa,
utajiri, na elimu kwa wenye nayo, kwa kutaja
machache yajulikanayo zaidi.
Kinachosisimua zaidi katika uchunguzi wangu
huu, nimegundua kuwa kuna baadhi ya watu ni
mashuhuri zaidi hata kuliko wengine wengi
wenye sifa hizo zilizotajwa hapo awali. Na
kwa bahati watu hawa hutokezea kuwa
hawakuwa na uluwa wowote rasmi, utajiri wala
Elimu ya kimagharibi kama ilivyozoeleka.
Katika rasimu hii nimejaribu kukusanya maoni
ya watu mbali mbali kisiwani Pemba kwa
kuwataka wanitajie watu wanaohisi ni mashuri
zaidi kisiwani humo. Nikataka pia umashuhuri
wao huo uwe umetokana na sababu zozote
zile zinazojulikana rasmi na nyenginezo
alimradi watu hao wapo katika hadhi fulani
ambapo ukiwataja tu wanajulikana na wengi
katika maeneo yao na hata nje ya maeneo yao
tena hata baada ya kufa kwao, kwa wale
waliokwishatangulia mbele ya haki. Na kwa
wachache walio hai bado majina yao hayahitaji
tochi kutambulika kutokana na umashuhuri
wao.
Kwa haya machache, natarajia kuwa
nimefahamika na naomba kwa heshima na
taadhima muniruhusu niwasilishe majina 40 ya
watu ambao nilitajiwa kuwa ni mashuhuri zaidi
katika maeneo mbali mbali ya Pemba. Ombi
langu kwenu, munipe maoni yenu kwa wingi.
Iwapo una mashaka na mmoja ya niliotajiwa
humu, basi niandikie uniambie. Nitafurahi zaidi
mkinipa michango yenye manufaa na pindipo
mkinikosoa kwa lugha nzuri na mkaniongoza
kwa pale nilipokosea, mchango wenu
nitauthamini na kuutambua rasmi katika kazi
hii.
Naomba niwatahadharishe tu, kuwa baadhi ya
majina ya watu yaliyoandikwa humu ni kwa
mujibu wa umaarufu wao na sio majina yao
halisi. Kwa kufanya hivyo, sina nia wala
makususdio ya kumchokoza wala kumdhihaki
yeyote kati ya walengwa hawa wala aila yake.
Na iwapo dhana hiyo itajitokeza na kuwaathiri
wegine, natanguliza kuomba radhi kwa kusema
‘kumradhi. Nambari za majina hazina maana
yoyote ya ubora au umashuhuri zaidi ya
wengine.
Naomba maoni yenu
Watu 40 Mashuhuri wa Kisiwa cha Pemba –
Rasimu ya kwanza ( kwa maoni na mjadala)
1. Ali Hemed – Raha,Gando
2. Ali Sultani Issa – Taifu, Wete
3. Babu Shiba – Kiuyu Mbuyuni
4. Bakari Pesa – Chambani
5. Baucha – Wete
6. Bavumo – Chwale, Madenjani
7. Bi Kirembo – Kiuyu Minungwini
8. Bi Mwamize – Mafya, Wingwi
9. Chondoma – Ziwani
10. Daudi Ngome – Maziwa Ng’ombe
11. Dimbo – Kiuyu Mbuyuni
12. Dr. Ali Mohammed Shein –Chokocho
Mkoani
13. Dr. Omar Ali Juma – Wawi
14. Hamad Kozi – Gando
15. Khamis Dondo – Shengejuu, Wimbini
16. Khamis Mwalimu – Wingwi
17. Kibano – Mtambwe
18. Kibichwa – Maziwa Ng’ombe
19. Kombo Ali ‘Kilozoni’ – Muambe
20. Mkamandume – Pujini
21. Muhammed Shamte Hamad – Mkanyageni
22. Muhunzi Faki ‘Kibora’ – Kojani
23. Mwinyi Ngushi – Msuka
24. Omar Bin Tumu – Kinowe
25. Othman Sharifu Mussa – Pandani
26. Prof. Said Ahmed Mohammed – Wete
27. Said Abeid – Fundo
28. Salim Ahmed Salim – Tundauwa, Mkoani
29. Seif Sharif Hamad – Nyali, Mtambwe
30. Shangiti – Micheweni
31. Sharifu Mwewe – Tumbe
32. Sheha Kidume – Ndagoni
33. Sheha Pembe – Chokocho
34. Sheha Subi – Ukutini
35. Sheikh Said Mana – Kiungoni, Shengejuu
36. Sheikh Alawi – Ole
37. Sheikh Habib Ali Kombo – Kangani,
Mkoani
38. Sheikh Nyange – Kangagani
39. Sheikh Qabi – Chake – Chake
40. Sheikh Suleiman Sharif – Tumbe

Historia ya mzee jumbe

Historia ya AL-HAJI ABOUD JUMBE MWINYI  Mwasisi wa serikali tatu Tanzania Na Yahya Abdullah Khamis (Yahya MAKAMO) Namfananisha Aboud Jumbe M...